Tuesday 8 June 2010

Nililia Kukeketwa

Leo naomba niwasimulie tukio hili la ukweli

Nilipokuwa na umri wa miaka sita (6) nilienda likizo kwa bibi yangu huko kijijini Buigiri mkoani Dodoma. Basi nikabahatika kupata marafiki wa nyumba za jirani watoto waliokuwa na umri kama wangu na wengine walikuwa wakubwa kwangu.

Baada ya siku kadhaa wenzangu sikuwaona tena, basi nikawa namsumbua bibi kuwa nataka kucheza na rafiki zangu, bibi naye akawa ananizungusha tu, sasa ikatokea siku moja bibi alikuwa anaenda kwenye kikao cha UWT kwani yeye alikuwa ni mwenyekiti hapo ikabidi anipeleke nyumbani kwa wale rafiki zangu, kufika huko doooohhh nilikuta wenzangu wamepakwa udongo mwili mzima, duh nikaona mambo si ndiyo haya bwana kuchezea udongo hadi hamu inaisha. Nami nikapakwa udongo halafu tukaanza kuimba na kunesanesa huku tumekaa chini tumenyoosha na kutanua miguu. Cha ajabu wale wenzangu wakawa hawana raha mara wanalalamika mara wanalia nilikuwa nawaona wazushi tu. Hatimaye mchana ukaisha, ipofika jioni bibi akaja kunichukua tukarudi nyumbani nikafurahi sana.

Baada ya siku kadhaa kukawa na tafrija kubwa sana kwa wale rafiki zangu kwa mara ya kwanza nikawaona wasafi na wamevaa nguo nzuri, kumbuka ni watoto wa kijijini tena wenye uwezo mdogo kifedha. Kulikuwa na ngoma sana na kijiji kizima kilikusanyika.

Ki-ukweli sikuelewa chochote katika umri ule, mpaka baadaye sana ndo nilipokuja kujua kuwa wale wenzangu walikuwa wamekeketwa!! Ndio maana walikuwa wakilalama na kulia wakati mwingine, kumbe walikuwa na maumivu masikini.

Dada mmoja kati ya hao waliokeketwa akaja kuishi Dar nyumbani kwetu baada ya kumaliza darasa la saba kama msaidizi wa ndani tuliishi naye kwa muda mrefu kiasi hatimaye akapata mume akaolewa, akabeba mimba lakini wakati wa kujifungua alifariki dunia na inasemekana kifo chake kilitokana na kuvuja damu nyingi kwasababu ya kovu la kukeketwa.

Masikini mimi nafikiria jinsi nilivyolilia ile hali ya kupakwa udongo na kuimba nikijua ni raha tupu kumbe wenzangu walikuwa wamefanyiwa ukatili wa hali ya juu.
Namshukuru sana bibi yangu (Mdala Rhoda Mwaka) kwa kuelemika kiasi cha kutojiingiza kwenye ukatili mkubwa namna hii kwa watoto wa kike. Bibi Pumzika kwa amani na mwanga wa milele ukuangazie huko uliko. Amina
Marehemu bibi yangu akiwa kambeba mwanangu wa pili Vicent

Kwa wakati ule ilikuwa mwezi wa sita (June) ni ngoma kila nyumba maana wavulana wanatahiriwa na wasichana hali kadhalika na wala haikuwa kwa kificho, ni wale tu ambao siyo wenyeji au wale walioelimika au wakristo safi ndio walikuwa hawawafanyii ukatili huo watoto wa kike.

Nikijiangalia leo nilivyo halafu ningekuwa nimenyofolewa kile kitu sijui ingekuwaje maana nasikia ukitolewa kile kitu raha ya ndoa inakuwa hakuna kabisa unakuwa msindikizaji tu.

Poleni wahanga wa ukeketaji



2 comments:

  1. Nani kakudanganya wewe kuwa wankakosa raha ya ndoa? Ungekuwa huk Mara mambo yangekuwa mswano tu ndugu yangu.

    Shukuru hukuolewa Ukuryani kwa kuwa siku ambayo mwanao wa kiume angetahiriwa na wewe ndo ungekeketwa hata walau sunna tu! Upo hapo?

    Anyway, hivo ni vijimambo tu!
    Ni kweli japo mie ni wa huko huko lakini sipendelei akina dada na wanawake kuondolewa 'gear box' kwani gari haitoenda :-(

    ReplyDelete